VIKWAZO VYA KUKUA KWA BIASHARA YAKO

mafingatown.blogspot.com




Hakuna kitu ambacho kinatokea bila sababu. Chochote unachoona kinatokea jua kuna kitu ambacho kimesababisha. Na hivyo kama unataka kubadili mambo yanayoendelea sasa ni lazima ujue sababu ilikuwa nini ili uweze kuidhibiti.
 
Hivi ndivyo ilivyo kwenye biashara pia. Kama biashara yako haifanyi vizuri sasa hivi sio ajali. Na wala sio kitu ambacho kimetokea tu kwa dharura, kuna vitu ambavyo vimesababisha biashara yako kutokufanya vizuri. Je ni vitu gani hivyo? 

Tatizo kubwa wafanyabiashara wengi huwa hawakai chini na kujiuliza swali hili pale mambo yanapokuwa magumu. Watu wengi hukimbilia kubadili baadhi ya vitu wanavyofikiri ndio tatizo na kushindwa kujua tatizo halisi limeanzia wapi. 

Hii ndio sababu kubwa inayowafanya wafanyabiashara kujikuta wanatumia fedha nyingi na wanaweka juhudi kubwa lakini hawaoni matokeo mazuri. Na mwishowe wanapojaribu kila kitu na kuona hakiendi vizuri anaishia kuamini labda kuna watu wamemfanyia vibaya na hata kuingiza imani za kishirikina. 

Kuendesha biashara kuna changamoto sana, kwa sababu biashara inahitaji muda wako mwingi na pia inahitaji umakini wako. Biashara yako inahitaji usimamizi na uongozi mzuri pia. Kama vyote hivi vinakuwa chini yako wewe mfanyabiashara, ni vigumu kupata muda wa kuitafakari biashara yako vizuri. Na hivyo unaweza kuona unaweka juhudi sana na unaweka fedha nyingi lakini huoni matokeo uliyoyategemea. 

Kuna maeneo sita muhimu ambayo yanaweza kuzuia biashara yako kukua. Wakati wowote ambapo biashara yako haifanyi vizuri yachunguze vizuri maeneo haya sita. 




1. Mzunguko wa fedha. 
Je mzunguko wako wa fedha upo vizuri? Je mauzo, manunuzi, matumizi na faida vinakwenda sawa? Je unaona ongezeko la thamani kwenye mtaji wako wa kibiashara? Kama mzunguko wa fedha una matatizo, biashara itaingia kwenye matatizo. 


2. Mauzo.
Je unauza kiasi cha kutosha? Je gharama zako za mauzo zinalipwa na faida inayopatikana na kisha ukabaki na faida ya ziada? Je kadiri siku zinavyokwenda mauzo yanaongezeka, yanapungua au yamebaki pale pale. Hili ni eneo muhimu la kuangalia kwa sababu ni kiashiria muhimu kama biashara inakua au inakufa. 


3. Masoko. 
Je biashara yako imewafikia wateja ambao ndio walengwa. Je soko la biashara yako umeshalifikia kwa kiasi gani? Linaongezeka au linapungua? Unatumia mbinu gani kutangaza biashara yako? 


4. Timu. 
Hii ni timu ambayo inafanya kazi kwenye biashara yako. Je umeajiri watu ambao wanapenda kufanya kazi wanayofanya? Je wanajituma? Je wanajua majukumu yao na kuyatekeleza kwa wakati na kwa ufanisi? Je wana ushirikiano mzuri? Kama timu yako haipo vizuri, basi italeta matatizo makubwa kwenye biashara yako. 
SOMA; Mambo matano muhimu kujua kuhusu wateja wako. 

                      


5. Matumizi ya rasilimali na muda.
Je matumizi ya rasilimali za biashara yako ni sahihi? Vipi kuhusu matumizi ya muda? Je umeweka kipaumbele kikubwa kwenye muda kutumika kwenye kazi za uzalishaji? Kama rasilimali na muda havitumiwi vizuri ni rahisi sana kupotea bila ya kuleta manufaa kwenye biashara. 







6. Huduma kwa wateja. 
Hii ni ya mwisho kwenye orodha hii ila ndio ya kwanza kabisa kwenye biashara yako. Kama huduma unazotoa kwa wateja wako ni mbovu basi jua biashara itashindwa kukua. Je wateja wanaridhishwa na huduma wanazozipata? Je wateja wanaifurahia biashara yako? Je wapo tayari kuwaambia wengine kuhusiana na biashara yako? Hayo ni baadhi ya maswali ambayo yatakuonesha kama unatoa huduma nzuri au la. 
Kila siku jiulize biashara yako inafanyaje kwenye maeneo hayo sita. Na utaweza kuzuia biashara yako kuingia kwenye matatizo na utaikuza zaidi na zaidi.


*haya ni baadhi ya mambo ya msingi ukiyafuata utafanikiwa kukuza biashara yako, achana na imani za ushirikina,mafanikio hayaji kama ndoto...




No comments:

Post a Comment